Bingwa wa dunia wa zamani wa masumbwi uzito wa juu, Mike ‘Iron’ Tyson amemchana bingwa wa zamani wa masumbwi, Floyd Mayweather kwa kauli yake kuwa yeye ni zaidi ya marehemu Muhammad Ali.
Mayweather alizua mjadala mzito mapema mwezi Januari mwaka huu baada ya kudai kuwa kutokana na rekodi yake ya kutopigwa hadi anastaafu masumbwi na namna anavyomudu mapambano, yeye ni zaidi ya Muhammad Ali kwenye karne hii.
Kupitia mahojiano aliyoyafanya hivi karibuni, Tyson amepinga vikali kauli ya Mayweather akidai kuwa ana hali ya ukichaa na kwamba ni muoga fulani mdogo asiyefaa kujilinganisha na Ali.
Tyson alidai kuwa kama Mayweather angekuwa ni mkali kuliko Ali, asingeweza kuwa anajificha macho ya watu hata kushindwa kuwapeleka watoto wake shuleni.
“Kama angekuwa hata angalau akaribia kuwa zaidi ya Ali, angekuwa na uwezo wa kuwapeleka watoto wake shuleni mwenyewe. Hawezi hata kuwapeleka watoto wake shuleni mwenyewe, na anazungumzia kuwa mahiri?” alihoji. “Umahiri sio kujilinda dhidi ya macho ya umma, umahiri ni namna unavyokubalika kwa watu,” alisema Tyson.
Alidai kuwa kuzungumzia umahiri zaidi ya Muhammad Ali sio sahihi, labda iwe kuzungumzia kuweka rekodi ya kutopigwa kwa sababu Ali aliwahi kupoteza mapambano kadhaa lakini Mayweather hajawahi kupoteza.