Kocha wa Arsenal Mikel Arteta amesema kujengwa upya kwa kikosi chake kipindi hiki cha majira haya ya joto kutawasaidia kushindana tena kuwania taji la Ligi Kuu ya England, lakini hilo pia lilifanywa kwa kurejea kwa nguvu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Arsenal waliongoza jedwali la Ligi Kuu ya England kwa muda mrefu wa msimu uliopita, lakini kikosi cha Arteta hakikuweza kuizuia Manchester City ya kocha, Pep Guardiola katika wiki za mwisho za msimu na kumaliza nafasi ya pili.
Licha ya kutoshinda taji la nyumbani, Arsenal ilipata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2016-17 hali ambayo ililazimu mabadiliko makubwa kwenye kikosi.
“Itakuwa ngumu zaidi kwa hakika, kwa sababu ligi itaenda kwa kiwango tofauti tena, ambayo tayari ni ya kushangaza,” alisema Arteta, ambaye alizungumza na ESPN huko Washington, D.C nchini Marekani, kabla ya mchezo wa timu yake dhidi ya MLS All-Stars jana Jumatano.
“Na ni wazi tuna hamu ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya ambayo hatujacheza kwa miaka mingi.
“Ndio maana tunahitaji kikosi tofauti na kile tulichokuwa nacho mwaka jana, nadhani tulichofanya msimu huu wa joto kinahusiana na hilo na ubora zaidi pia, bila shaka.”
Wachezaji wawili wakubwa walioongezwa Arsenal msimu huu wa joto ni kiungo Declan Rice na mshambuliaji Kai Havertz.
Arteta alimmwagia sifa zake Rice, ambaye alisajiliwa kutoka West Ham kwa ada ya rekodi na Havertz, mchezaji wa zamani wa Chelsea na Bayer Leverkusen.
“Havertz ni mchezaji ambaye nimekuwa nikimpenda kwa muda mrefu na tulikuwa na uwezekano wa kumleta klabuni.
Tulikuwa na mazungumzo machache kuhusu jinsi alivyokuwa anahisi kuhusu hilo na nilikuwa na hakika kwamba alikuwa aina ya mchezaji tuliyemtaka ili atupeleka mbele.”
“Rice analeta uongozi, analeta sifa maalum ambazo hatukuwa nazo kwenye safu yetu ya kiungo. Ni wazi, ana uzoefu mzuri kwenye ligi, tayari amefanya mengi akiwa na umri wa miaka 24, lakini ana kitu.”
Rice na Havertz wanajiunga na wachezaji wa kufurahisha pale Emirates akiwamo Bukayo Saka, Martin Odegaard na Gabriel Jesus, na Arteta aliongeza kuwa wachezaji wapya wa timu hiyo waliajiriwa sio tu kwa ajili ya vipaji vyao, bali pia kwa sababu walikuwa wanafaa kitamaduni kwa Arsenal.