Ligi Kuu ya England na kampuni inayosimamia waamuzi wa ligi hiyo, PGMOL imemweka kiporo Kocha Mikel Arteta kwa kitendo cha kuwashambulia waamuzi wa mechi ya Arsenal na Newcastle United hadi juma lijalo.
Kocha huyo wa Arsenal, alitoa matamshi makali kwa waamuzi baada ya timu yake kuchapwa 1-0 na Newcastle kwenye mchezo wa Ligi uliopigwa Jumamosi (Novemba 04).
Arteta alihoji uwezo wa mwamuzi Stuart Attwell pamoja na wale waliokuwa kwenye chumba cha VAR huko Stockley Park, wamewezaje kulikubali bao la Anthony Gordon lililokuwa pekee katika mnchezo huo.
Kinachoelezwa ni kwa kuwa Arteta hajawahi kuambiwa kwa tukio lolote la utovu wa nidhamu, hivyo suala lake linaweza kumalizwa kwa kupewa onyo kuliko kupigwa faini.
Mabosi wa Arsenal wametoa taarifa ya kumsapoti kocha wao kwa maneno aliyosema baada ya mechi hiyo ya Newcastle United.
Kipigo hicho cha Newcastle United kimewashusha Arsenal hadi kwenye nafasi ya nne ya msimamo wa Ligi Kuu England na kuvunja rekodi yao ya kutopoteza kwenye ligi hiyo tangu msimu ulipoanza.