Meneja wa Kikosi cha Arsenal, Mikel Arteta amesema tena kwa msisitizo hakuna hata mmoja kwenye kambi yake ambaye amekata tamaa kwenye mchaka mchaka wao wa kuufukuzia ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu 2022/23.
Manchester City imeiengua Arsenal kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu England baada ya ushindi wao wa mabao 2-1 dhidi ya Fulham juzi Jumapili.
Lakini, Arsenal inashuka uwanjani Emirates baadae usiku leo Jumanne (Mei 02) kukipiga na Chelsea na Arteta amesema: “Tunajua bado kuna kazi ya kufanya. Tumekuwa watulivu, tumejua udhaifu wetu na tumeifanya kazi kuwa bora uwanjani. Bado tuna nguvu na hilo limekuwa kama tabia kwenye kikosi chetu kwa miezi 10 iliyopita.”
“Kwa sasa ubingwa haupo kwenye mikono yetu. Kilichopo kwenye mikono yetu ni kujaribu kushinda kila mechi zilizobaki na mengine tutaiachia Man City. Sina kazi ya kuamsha ari ya wachezaji, wenyewe watawasha moto tu kwenye mechi hiyo. Ni ngumu kuitabiri Chelsea, lakini sisi tumejiandaa kushinda hiyo mechi.”
Arsenal ushindi wowote kwenye mechi hiyo dhidi ya Chelsea utawarudisha kileleni kwenye msimamo wa ligi licha ya kwamba watakuwa wamecheza mechi mbili zaidi ya mahasimu wao kwenye mbio za ubing- wa huo, Man City.
Takwimu zinaonyesha kwamba Arsenal na Chelsea zimekutana mara 61 kwenye Ligi Kuu England, huku chama la Mikel Arteta likishinda mara 24 katika mechi hizo, 14 ikiwa nyumbani na 10 ugenini, huku Chelsea, ambayo kwa sasa ipo chini ya Frank Lampard, imeshinda 20, mara 13 nyumbani na saba ugenini. Kuna mechi 17 zilizomalizika kwa sare.
Mechi tano zilizopita walizokutana wawili hao kwenye Ligi Kuu England, Arsenal imeshinda nne, ikiwamo ya kwanza msimu huu iliyofanyika Stamford Bridge, huku The Blues ikiwa imeshinda mara moja tu.
Kama takwimu zitajirudia, basi Arsenal huenda ikamvuruga akili Pep Guardiola kwa kuondolewa kileleni kama Arteta atashinda mechi yake.
Chelsea haijashinda mechi yoyote tangu Lampard arudi kuinoa timu hiyo.