Mtayarishaji mkongwe aliyewahi kutikisa mwanzoni mwa miaka ya 2000, Miikka Mwamba amefunguka kwa mara ya kwanza na kuelezea maajabu ya rapa ‘Balozi’ aka DolaSoul aliyewahi kutamba na wimbo wa ‘Kwenye Chati’.
Miikka Mwamba ambaye mikono yake iliwaibua wasanii kama Dully Sykes na ngoma zake ‘Julieta’, ‘Salome’ pamoja na albam nzito ya kundi la Daz Nundaz ‘Kamanda’, amesema kuwa Balozi alikuwa msanii wa Bongo Fleva aliyekuwa na uwezo wa ajabu wa kuingiza sauti mara moja tu akiwa studio na ukatoka wimbo mkubwa.
“Walikuwepo wasanii wanaoweza kufanya mara moja, lakini DolaSoul [Balozi] alikuwa na uwezo mkubwa sana wa kuingiza sauti mara moja tu yaani ‘take one’ na ukawa wimbo tayari,” Miikka Mwamba aliiambia Ayo TV.
“Kwa Mfano ile ‘Kwenye Chati’ aliingiza sauti mara moja tu na wimbo ukawa umekamilika,” aliongeza.
- HK Hyperman ‘kutia kachumbali’ ndoa ya Dulla Makabila na Husna
- Video: Ruby afunguka nje ndani kuhusu mpenzi wake mpya, ujio wake mpya
Kwa kawaida, wasanii wengi huingiza sauti mara kadhaa au kwa awamu kadhaa ili kukamilisha wimbo husika wanapokuwa studio, lakini kwa wasanii wengi wa zamani uwezo wa kukariri mashairi na kuyatema mfululizo ulikuwa unaangaliwa zaidi, kwa mujibu wa Miikka.
Mtayarishaji huyo wa Muziki ambaye ni raia wa Finland, amesema kuwa hivi sasa amepumzika kidogo kutayarisha muziki na anafanya kazi ya ukarimani nchini kwake akiwasaidia wasioelewa lugha ya Kiswahili kuelewana na wanaozungumza lugha hiyo.
Akiwa Tanzania, Miikka Mwamba alikuwa akifanya kazi chini ya FM Studio na alihusika kwa kiasi kikubwa kutayarisha albam ya kwanza ya Saida Kalori, ‘Maria Salome’ mwaka 2001.