Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuph Masauni, ameitaja mikoa mitano ambayo imekuwa na matukio yenye viashiria vya vitendo vya kigaidi ndani ya nchi, ikiwemo Geita na Arusha.
Masauni ametoa kauli hiyo, Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Azimio la Bunge la Kuridhia itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi huru za Afrika wa kuzuia na kupambana na ugaidi wa mwaka 2004, na kusema mikoa mingine ni Pwani, Tanga na Mwanza.
Amesema, sababu za vitendo hivyo ni dalili ya kuenea kwa itikadi za msimamo mkali zinazosababisha watu kuhamasika na kujiunga na vikundi vya kigaidi na vyenye misimamo mikali nje ya nchi, inayoweza kusababisha vitendo vya kigaidi nchini.
Katika azimio hilo, Tanzania itashirikiana na nchi jirani kulinda mipaka, kuanzisha Kituo cha Taifa cha kuratibu mapambano dhidi ya ugaidi ambacho kinaundwa na maofisa kutoka na vyombo vya ulinzi na usalama, huku Waziri Masauni akisema, “Tumekuwa tukitoa elimu kwa mikoa yenye viashiria vya kigaidi, ili wananchi wasishawishike kujiunga na vikundi au kufanya vitendo hivyo.”
Aidha, ameitaja itifaki hiyo kuwa ina vipengele muhimu ambavyo Tanzania imevizingatia ikiwemo malengo ya utekelezaji wa Ibara ya 21 ya Mkataba wa Umoja wa Nchi za Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi kwa matakwa ya mkataba husika.
Vipengele vingine, ni kuimarisha utekelezaji wa mkataba na kuwezesha utekelezaji wa itifaki ya kuanzishwa kwa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika katika kuratibu na kuoanisha jitihada za Umoja wa Afrika katika kuzuia na kupambana na ugaidi.
Alisema itifaki hiyo itawezesha Tanzania kubadilishana utaalamu na msaada wa kiufundi na kutumia kanzidata ya Kituo cha Afrika cha masuala ya ugaidi kilichopo Algiers, Algeria na kuanzisha vituo vya mawasiliano juu ya masuala ya ugaidi katika ngazi ya kanda.
Itifaki hiyo, inaeleza kuwa mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi wa mwaka 1999 utaweka utaratibu wa kisheria wa kubadilishana wahalifu kwa nchi ambazo hazina utaratibu huo.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Vita Kawawa alisema Itifaki hiyo ina tija kwa Tanzania ambayo si kisiwa kwa kuwa kumekuwa na matishio ya viashiria vya vitendo vya ugaidi ndani ya nchi.