Walimu wametakiwa kukopa kwenye Taasisi rasmi za kifedha ikiwemo Benki na kuachana na mikopo yenye riba kubwa maarufu kama kausha damu, na kuachana na mtindo huo mbovu wa maisha inayoathiri kipato chao na cha familia zao kwa ujumla.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga mjini Babati kwenye warsha ya Mwalimu Spesho iliyohusisha walimu 200 wa shule za msingi na Sekondari, huku mmoja wa walimu, Abdalah Hussein akisema walimu wengi wanakimbilia mikopo ya kausha damu kutokana na masharti nafuu.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema, “eneo kubwa lililoathirika na mikopo hii ni kada ya elimu na afya kwa kuweka bondi kadi zao za benki, tunapaswa kuachana na hayo kwani yanadhalilisha na kufedhehesha taaluma,” alisema Sendiga.
Hata hivyo, Mwalimu Hussein alisema elimu waliyoipata sasa itawanufaisha kwani walimu wengi wataondokana na mikopo umiza na kausha damu huku Meneja wa Benki ya NMB kitengo cha wateja Maalumu, Queen Kinyamagoha aliwaahidi walimu hao kuwapatia elimu ya fedha, ili watumie mikopo ipasavyo na kutimiza malengo yao.