Suala la Mila na Desturi nchini Tanzania bado lipo katika vichwa vya watu kwa baadhi ya Wanajamii kuamini kuwa Mwanamke ni chombo na wengi wao wakiwataka watoto wao wa kike kuandika majibu yasiyo sahihi katika mitihani yao ya mwisho, ili wafeli na hatimaye waje kuolewa kitu ambacho si sahihi kwani Mwanamke ni mama na anapaswa kuheshimiwa.
Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Fatma Tawfiq wakati akifanya mahojiano maalum na Dar24 Media hivi karibuni na kuongeza kuwa, hali hiyo imepelekea nafasi ya Mwanamke kuonekana si lolote mbele ya jamii licha ya matarajio yanayo chakatwa ya usawa wa 50 kwa 50 ifikapo mwaka 2050.
Amesema, “halafu wanaamini kwamba mtu anapokutolea mahari basi anaweza akakufanyia jinsi vile anavyotaka, mfano mtu katoa Ng’ombe 20 au 15 kwa ajili ya mahari anaona sasa huyu niliyemchukua ni wa kunifanyia kazi nyingi za kutosha kisa mila na desturi hili hapana.”
Aidha ameongeza kuwa, kinachotakiwa ni kupambana kuhakikisha dhana ya mila na desturi kwa baadhi ya mambo yasiyo na tija inatoweka, ili kuokoa mtazamo hasi dhidi ya Mwanamke na hatimaye kurudisha thamani ya utu kwake na kwa jamii kiujumla.