Mbunge wa Jimbo la Mchinga, Hamidu Bobali amedai kuwa alishawahi kushawishiwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa akijiunga na chama hicho atapatiwa kiasi cha shilingi milioni 200.
Ameyasema hayo visiwani Unguja katika mkutano wa Jumuiya ya Vijana wa Chama Cha Wananchi CUF ambapo pia mkutano huo ulihudhuriwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hammad.
Amesema kuwa viongozi wa CCM walimwambia wangeweza kumpa nafasi nyingine kwenye uongozi wa Chama cha Mapinduzi, madai ambayo Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humphrey Polepole ameyakanusha.
Aidha, amesema ujasiri ndio uliomfanya ashinde majaribu hayo, akibainisha kuwa mbali na mamilioni hayo aliyoahidiwa, pia aliahidiwa kuwa atateuliwa kuwa Naibu Waziri.
Hata hivyo, Mbunge huyo ameongeza kuwa kilichomfanya ashindwe kujiunga na CCM ni utu na uzalendo huku akiwashangaa wabunge wa upinzani waliohamia CCM kwa maelezo kuwa wamewasaliti wananchi waliowachagua.