Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 400 ndani ya mwaka wa fedha 2021/2022 kwaajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa daraja la kudumu katika mto Malagarasi litakalounganisha kijiji cha Ilagala na Kajeje, ikiwa ni mbadala wa kivuko cha Mv. Malagarasi ili kutatua changamoto ya usafiri na usafirishaji katika maeneo hayo.


Akizungumza na wananchi wa maeneo hayo wilayani Uvinza, mkoani Kigoma, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema kuwa  Serikali imeona adha wanayoipata wananchi wa hapo, na hivyo imeamua ndani ya mwaka huu  wa fedha kuanza mchakato wa ujenzi wa daraja hilo.

Aidha, Naibu Waziri Kasekenya, amemuagiza Kaimu Meneja wa Kivuko cha Mv. Malagarasi, Mhandisi Halfan Juma, kuhakikisha anaongeza muda wa utoaji huduma za usafirishaji unaotolewa Kivukoni hapo hususan katika kipindi cha kiangazi, kutoka  saa 12  asubuhi hadi saa 12 usiku kama ilivyokuwa awali na kusogezwa hadi saa Tatu usiku ili kuruhusu unafuu na urahisi kwa watumiaji wa huduma hiyo huku wakisubiri ujenzi wa daraja hilo.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kasekenya, amekagua barabara ya Simbo- Ilagala- Kalya (Km 231.29), ambapo  amesema kuwa ujenzi wa daraja hilo utaenda sambamba na uboreshaji wa barabara hiyo kutokana na umuhimu wake wa kusafirisha mazao mkoani Kigoma na nchi jirani za  Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Naye, Kaimu Meneja wa Kivuko cha Mv. Malagarasi, Mhandisi Halfan Juma, amesema kuwa ujio wa daraja katika maeneo hayo kutafungua fursa za kibiashara na uchumi katika wilaya hiyo na mkoa kwa ujumla.

RC Kunenge atoa onyo kwa wahalifu
Real Madrid kumnasa Mbappe?