Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameupa mnada wa Pugu Shilingi Milioni 600, kwa ajili kutengeneza eneo la kunyweshea mifugo maji, ambapo Mkandarasi ameshapatikana kwa ajili ya kazi hiyo itakayoanza wiki ijayo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega katika ziara yake ya siku moja kwenye mnada huo, ambapo amesikiliza kero za wafanyabiashara wa mnada huo moja ya changamoto ni utaratibu wa utoaji huduma katika mnada huo, uhaba wa maji, uchakavu wa miundombinu ya kuhifadhia mifugo na ubovu wa eneo la kushusha na kupakia mifugo.
Changamoto nyingine ni ukosefu wa taa ndani ya mnada, jambo ambalo Kaimu Mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam, Tabu Shaibu ameahidi kushughulikia ndani ya wiki moja.
Aidha wafanyabiashara wamemueleza Naibu Ulega, kuwa biashara katika mnada huo inaanza saa moja asubuhi, lakini changamoto wanayoipata ni suala la ukatishaji wa ushuru ambapo watumishi wanafungua ofisi saa tatu asubuhi kwa mujibu wa mwongozo wa minada.
Akifafanua juu ya utatuzi wa kero hizo Naibu Waziri Ulega amewaelekeza watendaji wa mifugo wa Wizara hiyo, kurekebisha mwongozo wa mnada ili kuruhusu shughuli za huduma kuanza saa moja asubuhi badala ya saa tatu asubuhi.
Ameongeza kuwa mwongozo huo uliwekwa wa saa tatu asubuhi kutokana na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu ambao wanaweza kufanya ujanja wa kwenda na mifugo katika minada kisha kuondoka nayo kwa kisingizio cha kukosa wateja na kuikosesha serikali mapato.
Amebainisha sababu nyingine kuwa ni upatikanaji wa huduma za kifedha kwa muda wa kuanzia saa moja asubuhi, hata hivyo amesema kitendo cha huduma hizo kuanza saa tatu badala ya saa moja asubuhi kinasababisha watanzania kukosa biashara kwa wale wanaotegemea mazao ya mifugo.
“Shusheni muda hadi saa moja asubuhi, ongeeni na watu wa mabenki waanze kutoa huduma kuanzia muda huo. Polisi wapo wana uwezo na uweledi wataimarisha ulinzi. Rais Samia Suluhu Hassan anapenda watu wafanye kazi na kulipa ushuru naagiza shusheni muda.” Amesema Mhe. Ulega.
Ameongeza kuwa kilichobaki ni miundombinu ya mabomba na mchakato utakamilika ndani ya wiki moja na kuhusu uzio kazi imeshaanza na amemuelekeza mkandarasi akamilishe kazi hiyo hadi Septemba 5 mwaka huu.