Serikali imetoa Shilingi milioni 700 kusaidia ukarabati wa barabara za vijijini katika jimbo la Karagwe mkoani Kagera ili kuboresha miundombinu ya jimbo hilo, hatua inayosaidia kurahisisha mawasiliano na kuboresha huduma za kijamii jimboni humo.
Akiwa katika ziara yake ya kukagua barabara inayokarabatiwa kwa kutumia fedha hizo, Mbunge wa jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ametaka fedha hizo zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.
Aidha Bashungwa amewahimiza wabunge wenzake mkoani Kagera kuwa mstari wa mbele kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili fedha iliyotolewa na Serikali kwa ajili ya kuboresha barabara za vijijini zifanye kazi iliyokusudiwa kufikia malengo ya kuwahudumia wananchi kwa kuboresha uchumi wao na taifa kwa ujumla.
Akizungumzia hatua hiyo meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA wilaya ya Karagwe Kalimbula Malimi amesema baada ya ziara hiyo sehemu zote zilizoainishwa ambazo zinahitaji marekebisho zitafanyia kazi haraka iwezekanavyo.
Ukarabati wa barabara hiyo unaanzia kata ya Nyakahanga kwenda kata za Nyabiyonza, Bweranyange, Nyakakika, Nyakabanga, Kibondo na Lukanja.
Wakati wa ziara yake, Bashungwa alifuatana na Madiwani wa kata mbalimbali, Watendaji wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na Watendaji wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS).
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi wa wilaya ya Karagwe akiwemo diwani wa kata ya Nyakakika Mhe. Exsavery Buguzi wameeleza matarajio yao kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutaongeza urahisi wa shughuli za biashara kwa maana ya usafiri na kusafirisha mizigo kati ya wakazi wa Mkoa wa Kagera na nchi jirani ya Rwanda kupitia kivuko cha Bweranyange ambacho kinaziunganisha nchi hizo mbili kwa usafiri wa majini.