Zaidi ya Waafrika milioni 91, wametajwa kuishi na Ugonjwa wa Homa ya Ini aina B au C, ambapo kwa ukanda wa Afrika mwaka 2020 pekee ulikuwa na asilimia 26 ya watu wanaougua maradhi hayo na kupelekea vifo 125,000 vilivyotokana na ugonjwa huo.
Taarifa ya WHO, kanda ya Afrika kutoka Brazaville nchini Congo imeeleza kuwa chapisho hilo la alama za Homa ya Ini kwa mwaka 2021, limeangazia takwimu kutoka kanda ya Afrika lakini limejikita katika Homa ya Ini aina B na C, ambazo husababisha ugonjwa wa cirrhosis na saratani au kansa.
Homa hiyo inatajwa kuwa mbaya zaidi ikilinganishwa na ile iliyochapishwa katika toleo la Julai 27, 2022 kwenye wavuti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni WHO, ambapo mwaka jana 2021 nchi 19 zilikuwa na zaidi ya asilimia 8 ya watu wameambukizwa homa ya ini na nchi 18 zikiwa na zaidi ya asilimia moja ya watu wanaoishi na homa ya ini.
Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika, Dkt. Motshidiso Moeti amesema asilimia 70 ya maambukizi ya Homa ya Ini aina B duniani kote hutokea barani Afrika na inaweza kuchukua miongo kadhaa baada ya kuambukizwa na virusi kabla ya mtu kuanza kudhihirisha dalili.
“Ni lazima tukomesha ugonjwa huu unaoiba maisha ya baadaye ya watoto wetu, kuna chanjo salama ambayo hutoa kinga kwa karibu asilimia 100 dhidi ya Homa ya Ini aina B ambayp ni mojawapo ya aina hatari zaidi za virusi,” amesema Dkt. Motshidiso.
Mkurugenzi huyu wa WHO amesema, “Ni lazima tuhakikishe kwamba watoto wote wa Kiafrika wanapata chanjo ndani ya saa 24 baada ya kuzaliwa na kufuatiwa na dozi mbili au zaidi za chanjo hiyo.” Amesema Mkuu huyo wa WHO kanda ya Afrika.”
Taarifa hiyo pia imeeeleza watoto milioni 4.5 wa Afrika wameambukizwa ugonjwa huo na takwimu za mpaka sasa nchi 33 zina maambukizi ya Homa ya ini aina B kwa zaidi ya asilimia 1, kati ya watoto walio na umri wa chini ya miaka 5, huku takwimu zikionesha maendeleo chanya ikilinganishwa na nchi 40 kwa mwaka 2019.
Uchunguzi uliofanywa na WHO, kuangalia maendeleo ya kati ya mwaka 2019 na 2021 umegundua kuwa chanjo ya kawaida ya watoto dhidi ya Homa ya Ini aina B ni asilimia 72 kwa Afrika ikiwa ni chini ya lengo la kimataifa la asilimia 90 linalohitajika.
Hata hivyo, Idadi ya nchi zenye chanjo ya zaidi ya asilimia 90 imeongezeka, kutoka nchi 23 mwaka 2019 hadi 27 mwaka 2021, wakati chanjo ya dozi ya kuzaliwa ikisimamiwa katika nchi 14 pekee za Afrika, na chanjo ya jumla ya asilimia 10 kwa ongezeko la nchi 11 kwa mwaka 2019.