Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amekasirishwa na ripoti ya wanafunzi 229 kupewa mimba mkoani Rukwa huku kukiwa na sintofahamu ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya wanaume waliofanya vitendo hivyo.
Akizungumza katika moja ya mikutano yake ya hadhara mkoani humo, Rais Magufuli ameonesha kushangazwa na idadi hiyo huku akiwanyooshea kidole viongozi wa mkoa huo.
“Kuna tatizo moja nimeliona kwenye mikoa hii ya Rukwa, mimba zimeongezeka. Mwaka 2018 watoto 229 wamepata mimba na sijasikia wanaume 229 wamefungwa zaidi ya miaka 30, na bado wanawatafuta wengine wawape mimba, wakati sheria zipo na Mkuu wa Mkoa yupo,”alisema Rais Magufuli.
“Serikali inatoa mchango kwa kutoa elimu bure na wanaume bure wanawapa mimba watoto wa shule! Hao wanaume bure 229 ndio viongozi? Kwa sababu kama sio hao viongozi, je viongozi wameshindwa kitu gani kuwapeleka hawa watoto kwenye haki?” Rais Magufuli alihoji.
Rais Magufuli aliwasihi viongozi wa dini kuingilia kati na kukemea vitendo hivyo, huku akiwaagiza viongozi wa Serikali kuhakikisha kuwa wanawalinda watoto wa kike dhidi ya ‘mafataki’. Alisema kama kuna mwanafunzi ana mimba kwenye eneo la kiongozi husika basi atambue kuwa hatoshi.
Aliwafunda pia wasichana katika mkoa huo wawape majibu magumu wanaume wanaotaka kuwadanganya ili wawape mimba.
“Ukiambiwa wewe mzuri mwambie akamwambie mama yake, msiogope kuwapa maneno magumu, nataka msome, nyinyi ndio marais wa kesho, mawaziri na wabunge. Hata kama mwalimu wako anakwambia anakupenda penda mwambie hayohayo majibu, takwimu za mimba mkoa huu zinatisha,”alisema Rais Magufuli.
Alisisitiza kuwa takwimu hizo ni aibu kwa mkoa wa Rukwa na zinakinzana na lengo la Serikali kutoa elimu bure hadi Sekondari ili kuwapa nafasi wasichana na wavulana kusoma na kujikomboa kimaisha.