Hatimae klabu ya Everton imekubali kutoa Pauni milioni 28.4 kwa ajili ya kumsajili beki wa kati wa mabingwa wa soka nchini Hispania FC Barcelona Yerry Mina, baada ya mazungumzo ya muda mrefu.
Klabu hizo zilikua katika mazungumzi kwa zaidi ya majuma mawili yaliyopita, huku ikiripotiwa Manchester United walijaribu kuingilia kati, lakini wamezidiwa kete na wababe hao wa Goodison Park.
Beki huyo kutoka nchini Colombia, ameafiki kuelekea Goodison Park, kwa kuamini ataweza kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, tofauti na Man Utd, ambapo huenda mambo yangemuendea kombo kutokana na mfumo wa meneja wa klabu hiyo Jose Mourinho.
Mina anadaiwa kukubali kujiunga na The Toffees kwa kuvutiwa na usajili wa aliyekua mchezaji mwenzake wa FC Barcelona Lucas Digne, ambaye tayari ameshatua klabuni hapo, akitanguliwa na wachezaji wengine Richarlison na Joao Virginia.
Beki huyo mwenye umri wa miaka 23, anatarajia kuondoka FC Barcelona wakati wowote juma hili, huku akiacha kumbukumbu ya kucheza katika michezo sita msimu uliopita, baada ya kusajiliwa mwezi Januari mwaka huu akitokea Palmeiras ya Brazil.
Kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara imekua sababu kubwa kwa beki huyo aliyekua miongoni mwa wachezaji waliounda kikosi cha Colombia wakati wa fainali za kombe la dunia nchini Urusi, kuondoka Camp Nou, katika kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi.
Baadhi ya vyombo vya habari vya England vinaeleza kuwa, huenda Mina akawa sehemu ya kikosi cha Everton katika mchezo wa kwanza wa ligi ya England mwishoni mwa juma hili dhidi ya Wolverhampton Wanderers, endapo atakamilisha kila hatua ya usajili wake juma hili.