Baada ya Simba kujihakikishia taji la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, kocha wa Ndanda FC, Meja Mstaafu wa Jeshi La Wananchi Tanzania (JWTZ) Abdul Mingange, amewamwagia sifa na kukiri walistahili kuwa mabingwa.

Mingange amesema Simba haijabahatisha kutwaa ubingwa huo, bali ilikuwa na vitu vilivyochangia mafanikio hayo kama uongozi imara, makocha wenye uwezo, wachezaji bora na uwanja wao wa mazoezi.

“Simba imestahili kutawazwa Mabingwa,wapo vizuri kuliko timu nyingine ambazo zinacheza Ligi Kuu Bara,ndio maana nimetaja vitu ambavyo vimewafikisha katika mafanikio hayo hawakubahatisha wala kupendelewa.

Mimi ni kocha sitaki kuongea propaganda za mashabiki, uwazi wangu utufunze kujipanga katika mambo muhimu yanayotakiwa katika soka, lengo tuwe na ushindani unaotakiwa ambao bingwa akipatikana anakuwa anafika mbali katika michuano ya kimataifa,”amesema.

Kuhusu uwezekano wa kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Mingange alisema kuwa wanaweza kufanya vizuri ikiwa watajiandaa vyema.

“Licha ya kwamba mwaka huu waliishia hatua za awali katika michuano ya CAF haina maana kwamba hawakuwa katika uwezo, isipokuwa naona wamepata funzo la kuweka umakini kwa kila mechi,”amesema Mingange.

Simba SC imetangaza ubingwa wa Tanzania Bara kwa kufikisha alama 79, huku ikisaliwa na michezo sita mkononi kukamilisha msimu 2019/20.

Mwishoni mwa juma hili mabingwa hao mara tatu mfululizo watasafiri hadi mjini Mtwara kucheza mchezo wa mzunguuko wa 33 dhidi ya Ndanda FC kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Messi aingia anga za Cristiano Ronald, afunga bao la 700
Fahamu maajabu ya Liverpool, Gundu la Klopp na Mane kwenda Madrid (Video)