Wakala wa kiungo kutoka nchini Ufaransa Paul Labile Pogba, ameweka hadharani maisha ya mchezaji wake ndani ya kikosi cha Manchester United, kwa kusema hana furaha kwa sasa.
Mino Raiola wakala wa kiungo huyo ambaye alirejea Manchester United mwaka 2016 kwa ada ya uhamisho ya Pauni milioni 89.3 sawa na Euro 105 (kwa wakati huo), akitokea kwa mabingwa wa soka Italia Juventus FC amesema Pogba hafurahii maisha ndani ya klabu hiyo inayonolewa na meneja kutoka nchini Norway Ole Gunnar Solskjær.
Amesema mchezaji wake amekua kimya na anashindwa kusema uhalisia wa mambo klabuni hapo, hasa baada ya kushindwa kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha Manchester United kwa kipindi cha miezi kadhaa.
“Hakuna sababu ya kuficha, ni bora kusema kwa uwazi, kuangalia mbele na kuepuka kupoteza muda. Paul hana furaha Manchester United, anashindwa kulisema hili kama ambavyo angetamani kufanya au watu wanavyotegemea angefanya. Anahitaji kubadilisha timu.” Amesema Mino Raiola akiiambia Tuttosport.
“Ana mkataba ambao utamalizika baada ya mwaka 1 na nusu (Majira ya kiangazi 2022), lakini suluhisho bora zaidi kwa pande zote ni kumuuza kwenye usajili ujao (Majira ya kiangazi 2021).”
“Tofauti na hapo klabu hiyo ya Old Trafford ambayo nina mahusiano mazuri, wanafahamu kuwa watakuwa hatiani kumkosa (Paul) kwa usajili huru ukizingatia kuwa kwa sasa mchezaji hana mpango wa kuongeza mkataba.”
“Kama kuna mtu asiyeelewa hili, basi anajua kidogo au hajui chochote kuhusu soka. Kwa vyovyote, wanaweza kuelekeza lawama zote kwangu kama Paul ataondoka kwenye usajili ujao.”
Paul Pogba ambaye alikuzwa kwenye kituo cha kulea na kuendeleza vijana cha Manchester United kuanzia mwaka 2009–2011 na badae kupandishwa kwenye kikosi cha kwanza, amekuwa kwenye wakati mgumu baada ya kupata majeruhi na kuathirika na virusi vya COVID19.
Kiwango cha Pogba kinaonekana kushuka maradufu akilinganishwa na alivyokuwa Juventus FC na miezi kadhaa ya mwanzo aliporudi Manchester United mwaka 2016. Maneno mengi yameshasemwa kama sababu za Pogba kushuka kiwango.
Kwa sasa, Pogba anasugua benchi na tangu Ole Gunnar Solskjaer alivyomsajili Bruno Fernandes. Pogba anaonekana kukosa namba ya kudumu kwenye kikosi cha meneja huyo ambaye anaonekana kuaminiwa sana na uongozi wa Manchester United.