Kocha wa Geita Gold FC Fred Felix Minziro ametamba kuendeleza moto wa kufanya vizuri katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuibanjua Ruvu Shooting mabao 2-1.
Minziro aliyeachiwa Mikoba ya Benchi la Ufundi baada ya kuondoka kwa Kocha Ettiene Ndayiragije amesema, kupata ushindi huo wa kwanza tangu wa Ligi Kuu, ni hatua nzuri kwa wachezaji wake, hivyo anaamini wataendelea kufanya kweli.
Amesema anaamini kilichokua kinasumbua kwenye kikosi cha Geita Gold FC ni kujiamini kwa wachezaji wake, lakini sasa hali hiyo imeshajikita kwa asilimia kubwa miongoni mwa wachezaji wake.
Pia usajili wa baadhi ya wachezaji kwenye kikosi cha klabu hiyo nao umeongeza chachu ya mapambano.
“Timu yangu sasa itaingia kwenye fomu ya kupata ushindi, kama ambavyo unajua nilichukua timu na tukapata michezo migumu tukiwa Dar es salaam. Tulivyorudi nyumbani pointi tatu zimepatikana.”
“Kuna wachezaji wapya wameingia kwenye timu, hilo nalo litaongeza kitu kwenye kikosi na naona sasa tunaenda kufanya vizuri kwenye michezo yote, tukianzia hapa kwetu, lazima tuondoke na alama tatu kwanza hapa,” amesema Minziro.
Geita wamecheza mechi nane, wakiwa na pointi tano, ushindi mechi moja, sare mbili na kufungwa michezo mitano.