Kocha mpya wa Tanzania Prisons, Fred Minziro amesema kwa mechi za kirafiki alizocheza ameona mabadiliko makubwa kwa wachezaji wake na anaamini watatoa ushindani mkubwa kwenye ligi.
Minziro amesema ushiriki wa timu hiyo kwenye mashindano ya ‘Samia Mbeya Nane Nane 2023’ kuona mwanga wa wa timu yake.
Amesema kwa sasa anarekebisha vitu vichache vya kiufundi na baada ya hapo watakuwa tayari kwa msinu mpya wa ligi kuu unaotarajiwa kuanza Agosti 15.
“Tumecheza zaidi ya mechi tatu za kirafiki zikiwemo zile za mashindano ya nane nane, kikosi naona kimeimarika lakini yapo mambo machache ambayo kwa siku hizi zilizobakia tutayafanyia kazi, naamini timu yangu itatoa ushindani mkubwa kwenye ligi,” amesema Minziro.
Amesema atapambana kuhakikisha timu yake inafanya vizuri zaidi msimu huu kwenye ligi tofauti na msimu uliopita ambao hawakufanya vizuri.
Katika mashindano ya ‘Samia Mbeya Nane Nane 2023’, Minziro licha ya kusaidia timu yake kuibuka mabingwa, pia alichaguliwa kuwa kocha bora wa michuano hiyo maalum.
“Haikuwa rahisi ilikuwa kazi ngumu lakini namshukuru mwenyezi mungu ameona ni jínsi gani Prisons tumejiandaa yote kwa yote kwa kuanza vizuri kazi kwenye timu hii,” amesema Minziro.
Mashindano hayo yalishirikisha timu nne za Prisons, Mbeya Kwanza, Mbeya City na wageni waalikwa Baka City kutoka Malawi ambao walishika nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Prisons.