“Bado nipo sana.” Ndio kauli iliyotolewa na Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Fred Felix Minziro’ mara baada ya kushuhudia timu hiyo ikipoteza tena kwa mabao 3-1 mbele ya Simba SC, akisema hajakata tamaa licha ya matokeo waliyonayo kwa sasa, kwa sababu bado kuna mechi kibao za kurekebisha makosa.

Hadi sasa ikiwa imeshacheza michezo minne, Prisons haijashinda mechi yoyote zaidi ya kutoka suluhu na Singida Fountain Gate na nyingine tatu kupigika, na kuifanya ishike mkia katika Ligi Kuu yenye timu l6.

Hata hivyo Minziro amesema hana presha kwani kwa sasa anajiandaa kwa mechi ijayo dhidi ya Mtibwa Sugar.

Minziro amesema wanaodhani amekata tamaa au kupewa muda kikosini wataendelea kusubiri sana akieleza kuwa bado anaendelea kufanya kazi yake kusuka timu ili kuhakikisha kwamba wanapata matokeo mazuri.

Amesema timu bora na imara inahitaji maandalizi ya muda mrefu akifafanua kuwa hata kutoanza vizuri msimu ni kutokana na ratiba waliyokutana nayo kwa kucheza na timu zilizomaliza msimu uliopita nafasi nne za juu.

“Ukiachana na Tabora United, tulikutana na Singida Big Stars na Azam zilizomaliza nafasi nne za juu msimu uliopita tukiwa ugenini, tunarudi Sokoine na Simba ilivomaliza nafasi ya pili, kibaya zaidi timu hii huwa haina ugeni, amesema Minziro.

“Hii va kusema nikate tamaa au kupewa mechi moja hakuna, bado nipo Prisons na ninaendelea kuisuka timu ili kuweza kupata matokeo mazuri na matarajio yangu mchezo ujao na Mtibwa Sugar tutashinda.”

Kocha huyo amekiri kwamba katika mechi ya Simba, vijana wake walifanya makosa ya kiufundi na kujikuta wakiadhibiwa akisisitiza kuwa ataendelea kurekebisha makosa ili kufikia malengo.

Pep Guardiola atoa angalizo kwa mashabiki
Mikutano itumike kukitangaza Kiswahili - Dkt. Ndumbaro