Kaimu Kocha Mkuu wa Geita Gold Fred Felix Minziro amesema kikosi chake kimekamilisha maandalizi ya kuelekea mchezo wa Mzunguuko wa saba wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo watakutana na Mabingwa watetezi Simba SC.
Kikosi cha Geita Gold kiliwasili jijini Dar es salaam mwishoni mwa juma lililopita, tayari kwa mchezo huo ambao utaunguruma kesho Jumatano (Desemba Mosi), Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kocha Minziro amesema wamefanya maandalizi ya kutosha kuelekea mchezo huo, ambao amekiri utakua mgumu kutokana na wenyeji wao kuwa kwenye mazingira ya kuhitaji ushindi kwenye uwanja wao wa nyumbani.
“Ninaamini mchezo utakua mgumu kutokana na wapinzani wetu Simba SC kuwa katika hitaji la ushindi, hata sisi tunahitaji ushindi na tutapambana, hivyo naamini mambo yatakua magumu kwa dakika zote 90.”
“Tunaiheshimu Simba SC kwa sababu ni timu kongwe na ina wachezaji wenye uzoefu, lakini kikosi changu kimejiandaa kikamilifu kupambana na hali hiyo, ninaamini kuna kitu tutakipata kwenye mchezo wa kesho.” amesema Minziro.
Simba SC ambayo bado haijapoteza mchezo wowote wa Ligi Kuu msimu huu, inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufikisha alama 14, ikitanguliwa na Young Africans yenye alama 16, huku Geita Gold ikishika nafasi ya 13 kwa kufikisha alama 5.