Uzinduzi wa miongozo minne ya Elimu ya Shule ya Nyumbani, ziara ya Nyumbani, upimaji na ubainishaji na uendeshaji wa Elimu maalum na jumuishi uliofanywa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda unalenga kuboresha utoaji wa elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum, ikiwamo kuwafuata majumbani.
Akizindua miongozo hiyo, jijini Dodoma, Prof. Mkenda amesema italeta mabadiliko chanya miongoni mwa wadau katika kutimiza azma ya serikali ya kuwapatia fursa ya elimu bora wanafunzi wenye mahitaji maalum nchini na kutoa wito kwa Viongozi, Wakuu wa Taasisi na Wadau kuendelea kushirikiana na Serikali kuhamasisha umuhimu wa elimu kwa watoto wenye mahitaji Maalum.
Amesema, “natoa rai kwa familia na wadau wa maendeleo waendelee kuona umuhimu wa kuchangia juhudi za serikali katika kuwapatia huduma stahiki wanafunzi wenye mahitaji maalum ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa ujifunzaji.”
Awali, Mkurugenzi wa Elimu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Susan Nussu alisema katika sensa waliyoifanya ya watoto wenye mahitaji maalum hadi Machi 2022 walikuwa 66,000 na zaidi ya 55,000 wapo Shule za Msingi na waliobaki wakiwa Sekondari.
Naye Mkurugenzi wa Elimu maalum wa Wizara hiyo, Dkt. Magreth Matonya amefafanua kuwa mwongozo wa shule ya nyumbani utasaidia kuhakikisha haachi nyuma mtoto yeyote kwenye upataji elimu na kwamba mwongozo wa ziara ya nyumbani utawasaidia walimu wanaokwenda ziara za nyumbani kupata taarifa zitakazowezesha kuchukua hatua stahiki.