Baada ya Droo ya African Football League kufanyika usiku wa Jumamosi (Septemba 02) na wawakilishi wa Tanzania katika mashindano hayo Simba SC kupangwa kuvaana na Mabingwa wa Soka Barani Afrika Al Ahly, staa wa zamani wa klabu hiyo ya nchini Misri aliyerejea Msimbazi, Jose Luis Miquissone ametamba kuwa amefurahi kupangwa dhidi mabosi wake wa zamani huku akiahidi atamuongoza Mnyama kuibuka na ushindi.
Droo ya mashindano hayo mapya ambayo yatafanyika kwa mara ya kwanza ilifanyika nchini Misri ambapo Simba SC watavaana na Al-Ahly Oktoba 20, mwaka huu na kurudiana nao Oktoba 24, mwaka huu.
Kama Simba SC watafanikiwa kufuzu nusu fainali ya mashindano hayo kwa kuwaondosha Al-Ahly basi wanatarajiwa kuvaana na mshindi wa mchezo kati ya Petro De Luanda ya Angola na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Akizungumza jijini Dar es salaam Luis amesema kwanza anajisikia furaha kuona wamepangwa timu ambayo anaifahamu vizuri kutokana na muda ambao amewahi kuichezea lakini pia hii itamkutanisha na marafiki zake wa zamani.
Ameongeza kuwa kila mchezaji yuko tayari kujitoa kuhakikisha wanashinda ubingwa wa mashindano hayo na mashindano mengine wanayoshiriki.
“Kama mchezaji kwanza nina furaha kubwa kurejea Simba SC, hii ni sehemu ambayo ilinipa mafanikio makubwa kabla ya kujiunga na Al-Ahly.
Bahati mbaya sana sikuweza kupata nafasi kubwa ya kucheza nikiwa na Al Ahly kwa kuwa na changamoto za majeraha, ila nimeanza vizuri hapa Simba SC na ninahamu ya kucheza dhidi ya rafiki zangu wa zamani (AI Ahly),” amesema Luis.