Kocha Mkuu wa Simba SC Robertinho amesema hana wasiwasi na Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Msumbuji Jose Luis Miquissone na tayari wameshamuandalia Programu maalumu.
Miquissone amesajiliwa Simba SC kwa mara ya pili akitokea Al Ahly iliyokubali kuvunja mkataba wa mchezaji huyo mwezi uliopita, kufuatia changamoto ya kukosa nafasi katika kikosi cha kwanza cha mabingwa hao wa kihistoria barani Afrika.
Kocha Robertinho amesema anaamini Kiungo huyo atakuwa msaada mkubwa sana katika kikosi chake kwa msimu huu 2023/24, hivyo amewataka Mashabiki kumpa muda.
Amesema Program aliyoiandaa kwa ajili ya Miquissone itamuwezesha kurudi katika kiwango na kasi yake ambayo ataitekeleza sambamba na wachezaji wenzake ambao walichelewa mazoezi ya maandalizi ya msimu mpya kule Uturuki.
“Luis ni mchezaji mzuri nampenda anajituma sana unajua bado ni mapema sana kumuona akifanya mambo makubwa, kuna mambo ambayo nilizungumza naye atahitaji muda kidogo kujirudisha kwenye ubora wake.
“Kitu bora ambacho watu wanatakiwa wafahamu huyu na mchezaji ambaye amerudi kuwatumikia Wanasimba anajituma sana ni mpambanaji na mshindani nidhamu hii itamrudisha haraka kwenye kiwango chake.
“Kuna Programu tumeitengeneza ambayo atafanya yeye na wenzake wote waliochelewa kambi ya Uturuki baada ya muda atakuwa sawasawa kucheza vizuri zaidi.” Amesema Robertinho
Miquissone jana Alhamis (Agosti 10) aliitumikia Simba SC katika mchezo wa Nusu Fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Singida Fountain Gate, huku akipiga moja ya mikwaju ya Panati iliyoiwezesha klabu hiyo kutinga Fainali.
Simba SC itacheza Fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Young Africans Jumapili (Agosti 13) katika Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga, saa moja usiku.