Imefahamika kuwa Kiungo Mshambuliaji wa Mabingwa wa kihistoria Barani Afrika Al Ahly, Luis Miquissone, yu njiani kurejea katika klabu yake ya zamani Simba SC, ili kuitumikia kwa msimu mpya wa 2023/24.
Taarifa kutoka ndani ya Simba SC zinaeleza kuwa, mpango wa kumrudisha Kiungo huyo kutoka nchini Msumbiji upo katika hatua nzuri na kama utapimwa katika asilimia basi upo katika asilimia 80, lakini kinachowavuruga viongozi wa Msimbazi ni maslahi binafsi ya mchezaji huyo ambaye alikuwa msaada mkubwa kabla hajaondoka Simba SC.
Hata hivyo bado kuna msisitizo kutoka kwa mabosi wakubwa ambao wanataka kuona nyota huyo anarudi Msimbazi kwa ajili ya kuwa sehemu ya kukiimarisha kikosi chao kuelekea michuano ya Super League, Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kwa sasa Miquissone hana nafasi ndani ya kikosi cha Al Ahly na tayari miamba hiyo imemweka sokoni nyota huyo baada ya mkataba wake wa mkopo wa kuichezea Klabu ya Abha inayoshiriki Ligi Kuu nchini Saudi Arabia kufikia tamati na kurejea kwao kwa sasa akifanya mazoezi binafsi.
Taarifa za uhakika zinasema kuwa uongozi wa Simba SC umelipitisha jina la Miquissone kwenye usajili wao mkubwa msimu ujao kupitia dirisha kubwa ambalo litafunguliwa hivi karibuni.
Taarifa hizo zimesema kuwa uongozi wa Simba uko katika mazungumzo na Al Ahly kwa ajili ya makubaliano maalum ili kuweza kupata huduma ya nyota huyo kutokana na masharti ya klabu hiyo kwa Miquissone.
“Miquissone kwa sasa hana nafasi tena katika kikosi cha Al Ahly ambao wanahitaji kumuuza lakini kutokana na dau kubwa waliloweka la kumnunua mchezaji huyo pia naye anataka mshahara wake ule ule unaofikia milioni 80 kwa mwezi, ambazo kwa hapa Tanzania ni ngumu kumlipa.
“Kwa kuwa tunahitaji huduma ya mchezaji huyo, tunafanya mazungumzo na Al Ahly ikiwezekana wao wawe wanamlipa asilimia 75 (milioni 60) katika mshahara wake na sisi Simba tutoe asilimia 25 (milioni 20),” zimeeleza taarifa kutoka ndani ya Simba SC
“Simba wana mpango wa kumrudisha Miquissone ndani ya timu hiyo na kuwa usajili wao mkubwa wakiamini wanaweza kumpata kutokana mahusiano mazuri baina yao na Al Ahly, kwa sasa wanatakiwa kukubaliana maombi hayo ili kuweza kupata huduma ya nyota huyo,” zimesisitiza taarifa kutoa Msimbazi.