Jumla ya miradi 74 Mkoani Kagera yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 18 inatarajiwa kuzinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi na mwenge wa uhuru katika wilaya nane za mkoa huo.

Miradi hiyo ya maendeleo katika sekta ya Afya, Elimu, Maji, Kilimo, Barabara, Ujasiriamali kwa watu wenye ulemavu, wanawake na vijana, viwanda na miradi 21. itazinduliwa, miradi 12 itawekewa mawe ya msingi na miradi 38 itatembelewa.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa mkoa wa Kagera Bregadia Jenerali Marco Gaguti wakati akitoa taarifa ya mapokezi ya Mwenge wa uhuru unaotarajiwa kupokelewa mkoani humo Aprili 24 mwaka huu katika kata ya Murusagamba wilaya ya Ngara.

Amesema kuwa ufanikishaji wa miradi hiyo umetokana michango ya sekta za umma, wahisani pamoja na Wananchi kwa viwango vya asilimia.

“kiasi cha pesa ambacho kimefanikisa miradi hiyo ni kutoka serikali kuu imechangia zaidi ya shilingi bilioni 10, sawa na asilimia 54, Halmashauri za wilaya na manispaa zimechangia zaidi ya milioni 282.8 sawa na asilimia 1.5 wahisani wamechangia zaidi ya bilioni 2 sawa na asilimia 13.9 na Wananchi zaidi ya Bilioni 5.8,”amesema Gaguti.

Aidha, amesema kuwa, kauli mbiu ya mbio za Mwenge wa uhuru kwa mwaka huu 2019 ni “Maji ni Haki ya kila Mtu tutunze vyanzo yake na tukumbuke kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa”

Hata hivyo, ameongeza kuwa kauli mbiu hiyo kwenye kipengele cha uchaguzi wa Serikali za mitaa, mkoa unatarajia kuandikisha Wananchi 1277776 watakao piga kura kwenye vituo 3798.