Tanzania bado ina mahitaji makubwa ya rasilimali fedha kutoka Baraza la Mfuko wa Mazingira wa Dunia – GEF, kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ambapo Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali yakiwemo mashirika ya kimataifa, ili kuhakikisha miradi ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira inaendelea kuibuliwa katika jamii.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa yanayofadhili miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi, inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Katika mazungumzo hayo, Jafo pia alipokea taarifa kutoka kwa wawakilishi hao kuhusu uwasilishaji wa andiko la taarifa la vipaumbele miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi itakayowasilishwa katika Baraza la Mfuko huo wa Mazingira wa Dunia, mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2023.
Amesema, mara baada ya kumalizika kwa kwa mkutano huo Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais iliunda timu ya wataalamu kwa ajili ya kupitia vipaumbele vya miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi kwa ajili ya uratibu wa maombi ya fedha za utekelezaji na usimamizi wa miradi hiyo.
“Tanzania ni mhanga mkubwa wa mabadiliko ya tabianchi. Leo ukitazama Wilaya ya Simanjiro utaona ni kwa jinsi gani wafugaji wanavyohangaika na mifugo ya. Na hata Mpwapwa napo hali nayo si nzu hivyo tunahitaji miradi mingi zaidi ya ufadhili wa fedha ili kuzinusuru jamii zetu,” amesema Waziri Jafo.
Kwa upande wake Mshauri wa Rais, masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira, Dkt. Richard Muyungi ameyashukuru mashirika hayo kwa kuendelea kufadhili miradi mbalimbali ya mazingira nchini na kuongeza kuwa, mahitaji makubwa zaidi ya fedha bado yanahitaji ili kuleta manufaa kwa jamii
na Taifa.