Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2021 hadi Januari, 2023 Serikali ilisajili jumla ya miradi ya uwekezaji 537 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 7,222.
Majaliwa, ameyasema hayo hii leo hii Aprili 20, 2023 wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa Kituo cha Biashara cha Afrika Mashariki, kinachojengwa na Kampuni ya East Africa Commercial and Logistics Center kwenye eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam.
Amesema, hatua hiyo imetokana na kuboreshwa kwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na kuimarisha Kituo cha Huduma za Mahala Pamoja ili kuvutia wawekezaji kwa kupunguza kero na kurahisisha utoaji huduma.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Majaliwa ameongeza kuwa ongezeko la usajili wa miradi hiyo unatarajia kutoa ajira takriban 92,770 kiwango ambacho ni kikubwa kuwahi kuandikishwa katika kipindi chochote tangu uhuru wa mwaka 1961.
Amesema, Serikali kupitia Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Mauzo ya Nje (EPZA) imefanikiwa kusajili Miradi 38 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 139.70 na mauzo nje yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 191.04.