Mshambuliaji wa mabingwa wa soka Tanzania bara Miraji Athuman ‘Sheva’ ambaye anashikilia rekodi ya kuwa ‘Super Sub’ wa kikosi cha mabingwa hao, msimu huu akiwa ameshikilia mabao ya Meddie Kagere amesema kuwa yupo fiti.
Sheva kabla ya kupata majeraha ya misuli na kifundo cha mguu (Enka) mwaka jana alipokuwa na timu ya Taifa ya Tanzania alionyesha maajabu kwenye ligi, akifunga mabao sita huku pasi yake moja na penati mbili alizosababisha mbele ya Mbeya City na Kagera Sugar zikifungwa na Kagere mwenye mabao 19.
Maajabu yote haya Sheva aliyafanya ndani ya dakika 508 alizocheza akiwa amehusika moja kwa moja kwenye mabao tisa ya Simba kati ya 63, akiwa na wastani wa kuwa na hatari langoni kila baada ya dakika 56.
Sheva amesema kuwa, anamshukuru Mungu ametenda maajabu kwani ameanza kurejea kwenye ubora wake.
“Ukweli napenda kumshukuru Mungu kwa kuwa nimeshaanza kurudi kwenye ubora wangu, naamini ligi ikianza nitakuwa moto,” amesema Sheva.
Michezo aliocheza ni tisa kati ya 28 ambayo alifanikiwa kutumbukiza mpira wavuni ilikuwa namna hii:- JKT Tanzania (30), Mtibwa Sugar (27) Kagera Sugar (29), Biashara United (83), Azam FC (33), Singida United (81), Mwadui (45), Mbeya City (90), Ruvu Shooting (90).
Muhimu: Namba zilizopo kwenye mabano ni dakika alizofunga mabao.