Kampuni ya ‘The Look’ iliyopewa dhamana ya kusimamia na kuratibu mashindano ya urimbwende ya Miss Tanzania yaliyokuwa yamesimamishwa, imesema imeyasuka upya ili kuyang’arisha.
Basila Mwanukuzi, aliyekuwa Miss Tanzania 1998, amesema kuwa kampuni yake ya The Look imeamua kufuta mashindano ya ngazi ya vitongoji ili kuondoa ubabaishaji uliokuwepo katika utoaji wa zawadi.
Amesema kuwa wamezifanyia kazi changamoto zilizokuwepo kwenye mashindano ya awali, ili kuhakikisha wawakilishi wa Tanzania wanang’ara katika mashindano ya Dunia.
“Haiweziekani Tanzania kwa miaka 10 katika mashindano ya dunia tumeshindwa kung’ara, lazima kuna tatizo mahali ambapo sisi sote tunatakiwa kulifanyia kazi,” alisema.
“Moja kati ya matatizo tunayotakiwa kuyafanyia kazi ni kuwaondoa watu wababaishaji ambao wamesababisha shindano limevunjiwa heshima yake,” aliongeza.
Miss Tanzania imerejea tena mwaka huu, baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe kulisimamisha mwaka jana na .
Dkt. Mwakyembe alichukua uamuzi huo kutokana na ubabaishaji wa wazi uliofanywa na waandaaji. Shindano hilo hivi sasa liko chini ya waandaaji wapya.