Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile ameiarifu Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuwa kiasi cha shilingi trilioni 18 zinapita kwenye mitandao kwa mwezi.
Ndugulile ameeleza hayo wakati wa kikao chake na kamati hiyo kilichohudhuriwa na wajumbe wa Menejimenti ya Wizara hiyo na wakuu wa taasisi zake ikiwemo Shirika la Posta Tanzania (TPC), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Baraza la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA -CCC) na Tume ya TEHAMA (ICTC) kilichofanyika kwenye ukumbi wa Bunge, Dodoma.
Ndugulile ameeleza kuwa kiasi cha miamala milioni 300 inafanyika kwa mwezi mtandaoni na Serikali inapata shilingi bilioni 80 za tozo kwa mwezi kutokana na mzunguko wa fedha mtandaoni kwa mwezi, akibainisha kuwa miamala inayofanyika na tozo ambazo Serikali inapata ni kutokana na kuwepo kwa matumizi ya TEHAMA.
Amefafanua kuwa Wizara hiyo imejipanga kuandaa ramani ya njia ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kufanikisha mwingiliano wa ujenzi na upanuzi wake pale inapokutana na njia za miundombinu mingine kama vile ya barabara, maji, umeme na reli.
Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Moshi Kakoso ameitaka Wizara hiyo kuongeza udhibiti na usimamizi wa huduma za mawasiliano kwenye suala la fedha mtandao ili kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha na kuweza kuongeza mchango wa tozo Serikalini zaidi ya shilingi bilioni 80 kwa mwezi.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula amewaeleza wajumbe wa Kamati hiyo kuwa Wizara itaendelea kusimamia na kuendesha vema Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaendelea kunufaika na huduma za mawasiliano na TEHAMA
inatumika kurahisisha maisha yao ya kila siku katika nyanja ya kiuchumi na kijamii.