Kuboreshwa kwa miundombinu kumetajwa kusaidia kwa kiasi kikubwa huduma ya damu salama kwenye Kanda ya Magharibi ambayo inahudumia mikoa ya Tabora,Katavi,Singida na Kigoma.

Hilo limebainishwa na Kaimu Meneja wa kanda hiyo Zaituni Abdalah wakati wa kampeni ya kukusanya damu kwenye shule ya sekondari Mabama iliyoko Manispaa ya Tabora.

“Kwa kiasi kikubwa uboreshwaji wa barabara umesaidia sana kurahisisha upatikanaji wa mahitaji wa damu salama kwenye mikoa hii tunayoihudumia ambayo inayo eneo kubwa kijiografia hivyo inapohitajika damu kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma tunawapatia kwa wakati” amesema Zaituni.

Kaimu Meneja huyo amesema katika wiki hii ya kampeni ya kukusanya damu iliyoanza tarehe 21 mwezi huu ambayo itamalizika tarehe 25, kanda yake imeweza kukusanya chupa 186 kwa siku mbili ikiwa imekaribia lengo lililoweka la kukusanya chupa 100 kwa siku na chupa 500 zinazotarajiwa kukusanywa kwa wiki.

“Kama kanda hatujachoka kuhamasisha wananchi licha ya changamoto ya uelewa kwa jamii kuhusu uchangiaji damu,hivyo tumejipanga kuendelea kutoa elimu kwenye makundi yote ili tuweze kuwa na damu za kutosha kwenye hospitali zetu” ameongeza Zaituni.

Kama Kauli mbiu ya kampeni hiyo inavyosema “changia damu,ili kuokoa maisha ya akina mama wanaoleta uhai duniani “ jamii imeaswa kuchangia damu mara kwa mara ni muhimu ili kuokoa vifo vya akina mama wajawazito wanapoteza uhai wakati wanapojifungua.

Naye Afisa Mhamasishaji wa kanda hiyo Constantine Chiba amesema wamejiwekea utaratibu kutoa elimu ya kuchangia damu kwa kutembelea vijiji mbalimbali ,nyumba za ibada pamoja na makundio mengine katika jamii ili kuweza kuwa na akiba ya damu na pindi inapohitajika .

Chiba ametaja makundi matano ya wahitaji wa damu yakiwemo wajawazito na watoto wachanga,wahanga wa ajali, wanaohitaji tiba ya upasuaji,wenye matatizo ya kuishiwa damu (sikoseli) na kundi la mwisho ni watu wote ambao wanaweza kuugua na kuhitajika kuongezewa damu.

“Kumbe sisi sote ni wahitaji wa damu kwani hatuwezi kuyakwepa makundi haya yote kama binadamu, kwani ugonjwa au ajali haiwezi kukwepa jinsia au umri wa mtu” amesema Chiba.

Alexei Navalny aruhusiiwa hospitali
Lissu: Tutabadilisha mfumo wa kiutawala