Hospitali ya Kairuki imefunguliwa shitaka na kutozwa faini ya shilingi milioni 155 kutokana na uzembe uliofanywa na daktari wakati wa upasuaji na kusahau pamba ndani ya mfuko wa uzazi wa mkazi mmoja wa Dar anayejulikana kwa jina la Hyairat, hali iliyopelekea mama huyo kuondolewa kizazi na kupata tatizo la Fistula.
Khairat kupitia Kampuni ya Uwakili ya Jonas amefungua kesi ya madai namba 184 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Khairat amedai kuwa amekuwa akihudhuria kliniki wakati wa ujauzito katika hospitali ya Kairuki, Desemba 15 mwaka jana alijifungua kwa upasuaji na karuhusiwa Desemba 17 mwaka huo na kutakiwa kurudi tena Desemba 21.
Aidha amesema kuwa alianza kusikia maumivu akiwa nyumbani kwake na mnamo Desemba 21 alirudi hospitali kumuona daktari kueleza maumivu anayopata na kuomba afanyiwe Ultra Sound.
“Akiwa nyumbani hali iliendelea kuwa mbaya, alisikia maumivu makali ya kichwa na alianza kubadilika rangi ambapo alikimbizwa hospitali ya jirani, walipompima wakaelekeza apelekwe Regency Hospital kwa matibabu zaidi.
“Regency walimfanyia vipimo na kubaini kuna tatizo katika mfuko wa uzazi na kumuhamishia Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako pia walimfanyia vipimo na kubaini wakati alipofanyiwa upasuaji kuna vitu vilibakia kama pamba ambavyo vimesababisha mfuko wa uzazi kuharibika,” ilisema sehemu ya hati hiyo ya madai.
Pia amesema kutokana na uzembe na kutokuwa makini wakati wa kumzalisha ameomba mahakama iamuru alipwe Sh milioni 20 gharama za matibabu, Sh milioni 25 fidia kwa kukosa kipato wakati anaumwa, Sh milioni 80 gharama za adhabu na Sh milioni 30 fidia.
Wadaiwa wanatakiwa kupeleka utetezi wao mahakamani na kesi hiyo itatajwa Agost 31, mwaka huu.