Yussuf Yurary Poulsen ni mchezaji ambaye baba yake ni Mtanzania na ameitwa katika kikosi cha wachezaji watakaoiwakilisha Denmark katika michuano ya kombe la Dunia nchini Urusi.

Poulsen alizaliwa mwaka 1994 huko Copenhagen Denmark, babake alikuwa anafanya kazi kwenye meli ya makontena iliyokuwa inatoka nchi za Afrika kwenda Denmark na katika moja ya safari hizo ndipo alikutana na mama wa mchezaji huyo anayeitwa Lane raia wa Denmark.

Baba mzazi wa mchezaji huyo alifariki kutokana na kansa mchezaji huyo alipokuwa na umri wa miaka sita lakini Poulsen amekuwa akija Tanzania mara kadhaa kumtembelea bibi yake jijini Tanga.

Poulsen anacheza soka la kulipwa katika klabu RB Leipzig inayocheza ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga. Anacheza nafasi ya ushambuliaji, anavaa jezi namba 9 na amewachezea Leipzig jumla ya mechi 156 na kuwafungia mabao 37.

Mchezaji huyo amezaliwa na kukulia Denmark na amecheza timu zote za vijana za Denmark na sasa timu ya wakubwa, hakuwahi kupata ofa yoyote ya kuichezea timu ya taifa ya Tanzania iwapo atachezeshwa katika kikosi cha Denmark basi atakuwa mchezaji wa kwanza wa asili ya Tanzania kucheza katika fainali za Kombe la Dunia

Klabu nyingi za Ulaya kama Wolfsburg na Borussia Monchengladbach zimeonesha nia ya kumnunua na mchezaji huyo anatumai kwamba kucheza katika Kombe la Dunia kutamfanya kufahamika zaidi Ulaya.

 

 

Video: Huu ni ukatili, huwezi kumuua mwenzio kwa wivu wa mapenzi- Dkt. Bisimba
Hector Cuper atoa somo la saikologia kwa wachezaji wa Misri