Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) NEC, Jafari Kubecha ameeleza kuwa miongoni mwa mafunzo makubwa aliyotuachia aliyekuwa Rais wa Tano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Magufuli ni suala la udhaifu wa kimwili kwa magonjwa au udhaifu wowote ule kutokuwa tija ya kumfanya mtu kutokufanya kazi kwa madhubuti.
Kubecha ameeleza hayo katika kipindi cha mahojiano na Dar24 Media kuhusiana na kifo cha hayati Dkt. Magufuli ambapo amesema kuwa Dkt. Magufuli alitufunza kuwa imara, jasiri na kuwa wazalendo na hata kwa bara la Afrika kuwa na ujasiri wa kuona likiamua kila jambo bila kuwa na hofu basi linawezekana.
Aidha ameongeza kuwa Magufuli amefariki akiwa na malengo makubwa ya maendeleo kwa ya Tanzania.
Akizungumza kuhusu aliyoyafanya Hayati Dkt. Magufuli kwa Chama cha Mapinduzi, Kubecha amesema hayati Magufuli alifaulu kusimamia mafanikio ya kiuongozi na kufanya chama kuwa na misingi imara, hata kuunda tume ya makinikia ya kuchunguza mali za chama na kuweka misingi bora.
Amesema kuwa wakati wote enzi za uhai wake na kama Mwenyekiti wa Chama hicho, Dkt. Magufuli alikuwa mtu wa kuusia sana umoja, mshikamamno, haki, usawa na uchapaji kazi kwa ujumla.