Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Young Africans Alex Ngai amekanusha taarifa za Klabu hiyo kuwa mbioni kumtimua kazi Kocha Mkuu Nasreddin Nabi.
Mapema leo Jumanne (Oktoba 25) Gazeti la Mwanaspoti limeripoti Kocha huyo kutoka nchini Tunisia yupo njiani kutimuliwa, huku Kocha kutoka Brazil na Klabu Bingwa nchini Uganda Vipers SC Roberto Oliveira Gonçalves do Carmo.
Ngai amesema amesikia na kuona taarifa za Young Africans za Kocha Nabi kuwa mbioni kutimuliwa, lakini ukweli ni kwamba Kocha huyo bado yupo na anaendelea na majukumu yake.
Hata hivyo Ngai amesema hata ikitokea Kocha Nabi ameondoka, Young Africans haitabadilika, kwani imewahi kuwa na viongozi wengi na makocha wengi na waliondoka.
“Nabi bado ni Kocha Mkuu Young Africans na hapa Young Africans wamepita watu wengi, alikuwepo Tabu Mangala lakini leo tuko sisi na Rais wetu Hersi Said, hivyo hata akiondoka bado hakuna kitu cha kushangaza.” amesema Ngai
Kocha Nabi anayeshikilia Rekodi ya kuingoza Young Africans bila kufungwa tangu msimu uliopita, anatajwa kuwa mbioni kuondoka klabuni hapo, kufuatia kushindwa kuifikisha klabu hiyo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Young Africans iliondolewa kwenye Michuano hiyo kwa kufungwa na Al Hilal ya Sudan 2-1.