Aliyekua mkaguzi wa chakula cha Rais Mzee Abdalah Chasamba amezitaja sababu za yeye na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuwa marafiki hadi kupewa hadhi ya ukaguzi wa chakula cha Rais Ikulu, ambapo amesema wote walikuwa na nia ya kuhakikisha Tanganyika kujipatia uhuru wake.
Chasamba ameyasema hayo wakati akizungumza na Dar24 Media katika mahojiano maalumu na kueleza kuwa Baba yake alichangia kwa kiasi kikubwa yeye kushirikiana na Chama cha TAA kupambania uhuru.
Amesema, “Mwalimu Nyerere baada ya kuanzisha chama cha TAA hapa Dar es Salaam alitoka kwenda Morogoro kwa Chifu Kambi Gungulugwa, kwa ajili ya kupata msaada wa kuwashawishi vijana kujiunga na chama na alifanikiwa na nilijiunga kisha kwenda Dar es Salaam.”
“Nilienda makao makuu ya TANU na nilipofika nikamkuta Pius Msekwa ndiyo alikuwa katibu mkuu TAA wakati huo na nikamwambia kuwa nimeona nije hapa niungane na Nyerere kitu anachodai uhuru hata mimi kinanikwaza kwanini tutawaliwe na hawa wazungu kwanini tusijitawale wenyewe miaka yote hiyo na akanipeleka hadi kwa Nyerere,” alisimulia Mzee Chasamba.
Aidha amesema, Msekwa ndiye aliyemkutanisha na Nyerere na akamueleza dhamira yake ya kutaka kuonana naye na alimkubuka baada ya kumueleza kuwa pale alipofikia akiwa Morogoro kwa Kambi Gungulugwa ni kwa baba yake na hivyo mwanzo wa mahusiano yao na harakati za kupigania uhuru zilianzia hapo.