Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajia kupanga mikakati ya kuendeleza Sekta ya Sheria nchini kwa ajili ya kuwatumikia watanzania.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende ameyasema hayo wakati akitoa salamu kwenye kikao kazi cha Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo vya Sheria wa kutoka Wizara mbalimbali, Taasisi za Serikali, Mashirika ya Umma na Halmashauri zote nchini.
Amesema, kupitia kikao hicho chenye kauli mbiu isemayo, “Utekelezaji wa Majukumu Unaozingatia Sheria ni Nyenzo Muhimu kwa Maendeleo ya Taifa,” wanalenga kupanga mikakati ya kuendeleza Sekta pamoja na kubadilishana uzoefu ili kupata wanasheria wabobezi ndani ya Serikali na kuisaidia Serikali kutekeleza majukumu yake.
Awali, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Dkt. Eliezer Feleshi alisema viongozi hao wanatakiwa kuelewa dira na dhima ya Ofisi wanazotumikia kwa kufanya tathmini, kujipima namna wanavyotekeleza majukumu na kufanya uchambuzi wa wadau wa ndani na nje ya taasisi wanayofanyia kazi.
Ameongeza kuwa, pia wanatakiwa kuweka mikakati endelevu ya kujengeana uwezo, kuepuka kujenga uadui na makundi, kufurahia kukoselewa na kufanyia kazi maeneo waliyokosolewa na kuwa wadilifu ili wawe na nguvu ya kuchukua hatua.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi waliotoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Shaban Ramadhan Abdallah, amesema kupitia mafunzo hayo wamejifunza kutekeleza ushirikiano baina ya Ofisi hiyo ya SMZ na za Tanzania Bara.