Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewasilisha mpango mkakati wa kipindi cha miaka mitano kwa ajili ya kuendeleza sekta za mifugo na uvuvi ili kuinua zaidi mchango wa sekta hizo katika pato la taifa ifikapo mwaka 2025/26.
Mpango mkakati huo umewasilishwa mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji ambapo katika sekta ya mifugo mpango huo mbali na mambo mengine umekusudia kukuza tasnia za nyama na maziwa.
Akizungumza mbele ya kamati hiyo, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Amosy Zephania amesema mpango huo umezingatia kanda mbalimbali nchini ambazo zimekuwa zikifanya vizuri katika tasnia hizo ili kuwekeza zaidi kwenye maeneo hayo ili kupunguza gharama za uzalishaji.
Amesema ni muhimu tasnia za maziwa na nyama ambazo ndiyo maeneo ya kimkakati kuwekewa nguvu zaidi ili uzalishaji umnufaishe mfugaji wa chini ambaye ndiye mlengwa na kuwa na uchumi jumuishi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amesema mpango mkakati wa kuendeleza sekta ya uvuvi utajumuisha sekta binafsi na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha sekta hiyo inakuwa na tija zaidi kwa nchi na mwananchi mmoja mmoja.
Amefafanua kuwa katika mpango huo kwenye kipindi cha miaka mitano unalenga kuhakikisha mapato yanaongezeka na kuifanya sekta ya uvuvi kuongeza tija zaidi katika pato la taifa.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Dkt. Christine Ishengoma amesema mpango mkakati wa kuendeleza sekta za mifugo na uvuvi wa kipindi cha miaka mitano ni vyema elimu zaidi iendelee kutolewa kwa kushirisha maafisa ugani.
Dkt. Ishengoma ameongeza kuwa ana imani mkakati huo ukifanyiwa kazi na kutekelezwa utaleta tija kwa taifa hususan kwa wafugaji na wavuvi.