Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Benjamini William Mkapa amesema ipo haja ya kuitishwa mjadala wa kitaifa wa kujadili hali ya elimu nchini kufuatia shule za serikali kuendelea kufanya vibaya katika matokeo ya mitihani ya kitaifa.
Mkapa ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma amesema hayo mkoani Dodoma wakati wa tukio la kumkaribisha kazini Makamu Mkuu mpya wa chuo kikuu cha Dodoma Profesa Egid Mubofu na kumuaga Makamu Mkuu wa chuo hicho aliyemaliza muda wake Profesa Idrisa Kikula.
Mkapa amesema mjadala huo unatakiwa kuhusisha makundi yote ya jamii bila kujali kama ni ya sekta binafsi ama ya umma sambamba na watu wa kawaida siyo wasomi pekee ambapo kupitia njia hiyo anaamini suluhu ya kudumu itapatikana.
Mkapa amezungumza hayo kufuatia na mfululizo wa matokeo mabaya katika mitihani ya kitaifa, ambapo hali hiyo ni tofauti na zamani, siku hizi ni adimu sana kwa shule za Serikali kama Kibaha, Mzumbe, Pugu, Jangwani na nyinginezo kushika nafasi za juu kumi bora kama ilivyokuwa zamani.
Kwani nafasi hizo kwa zama hizi zimekuwa zikishikwa na shule binafsi ambazo kwa mfululizo wa zaidi ya miaka mitatu zimekuwa ziongoza huku shule kumi za mwisho zote zikiwa zinatoka serikalini.