Serikali nchini, imejipanga katika kuhakikisha inakuwa na miundombinu bora ya mawasiliano yenye kutumia teknolojia ya kisasa ambayo italeta tija na ufanisi katika kuongeza uzalishaji na ujenzi wa uchumi pamoja na kuimarisha usalama na ulinzi wa Taifa.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, ameyasema hayo hii leo Aprili 17, 2023 jijini Dodoma katika hafla ya utiaji saini kati ya TTCL na Kampuni ya HUWAWEI kuhusu upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika Wilaya 23.
Amesema, “tutahakikisha Mkongo huu wa Taifa unafika katika ngazi ya Mkoa, Wilaya na katika mipaka ya Nchi yetu, na Mikoa Yote Nchi nzima imeshaunganishwa katika Mkongo wa Taifa na Mkongo umefika katika vituo vya mipakani ambavyo vimepakana na Nchi Jirani.”
“Serikali inafanya juhudi kubwa kupitia Wizara ya habari , Mawasiliano na Teknolojia ya habari katika kuimarisha sekta ya Mawasiliano.ivyo tutaifanya Tanzania kuwa Nchi muhimu katika ukanda huu wa Afrika mashariki na Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika,” amesema Nape.
Aidha ameongeza kuwa, Serikali katika kutambua changamoto za Wilaya ambazo zimekosa mawasiliano ya uhakika ambayo yamesababisha Wananchi kukosa fursa katika Wilaya zao.
“Katika kutatua changamoto hiyo Serikali imejipanga kutekeleza mradi wa kuimarisha mawasiliano katika ngazi ya Wilaya kwa kuunganisha Wilaya zote kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kuongeza kasi ya upatikanaji wa Mawasiliano ambayo yatachochea maendeleo katika Wilaya hizo na Taifa kwa ujumla,” amesema Nape.