Klabu ya Arsenal itasaini mkataba na kampuni ya vifaa vya michezo ya Adidas na kuachana na kampuni ya Puma kuanzia mwaka 2019.
Mkataba wa kampuni ya Puma uliokua unaiingizia klabu hiyo Pauni milioni 30 kwa mwaka utafikia kikomo mwanzoni mwa mwaka ujao, na kampuni ya Adidas imeonyesha kuwa tayari kusaini mkataba na klabu hiyo ya jijini London, ambao utakua na thamani ya Pauni milioni 60 kwa mwaka.
Mkataba wa Adidas ambao utakua na thamani mara mbili zaidi ya Puma, unatarajiwa kuwa wa miaka mitano, na utamsaidia meneja mpya wa klabu hiyo Unai Emery kufanya usajili wa wachezaji wakati wa dirisha dogo la usajili, mwezi Januari.
Kwa sasa meneja huyo kutoka nchini Hispania ameshatumia zaidi ya Pauni milioni 70, kufanya usajili na ameshindwa kuendelea kuleta wachezaji wapya klabuni hapo, kutokana na bajeti yake kufikia kikomo.
Uongozi umeshamuarifu kufanya utaratibu za kuuza baadhi ya wachezaji ili kupata fedha za kusajili wengine, kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili kesho Alkhamis.
Kiungo Aaron Ramsey anatazamwa kama sehemu ya kupatikana kwa fedha za usajili katika kipindi hiki, na tayari Chelsea wameonyesha nia ya kumsajili kwa ada ya Pauni milioni 30.
Kiungo huyo yupo kwenye hati hati ya kuondoka Emirates Stadium, kufuatia mkataba wake kuwa mbioni kufikia kikomo, na kama hatosaini mkataba mpya, mwishoni mwa msimu wa 2018/19, ataondoka kama mchezaji huru.
Endapo Arsenal watafanya kosa hilo, watarudia walichokifanya kwa mshambuliaji Robin van Persie ambaye aliondoka klabuni hapo mwaka 2012, na kujiunga na Manchester United kwa ada ya Pauni milioni 22.5, baada ya kugoma kusaini mkataba mpya.