Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limeridhia Tanzania kujiunga na Mkataba wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu – IRENA kufuatia Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko kuwasilisha azimio hilo Bungeni.
Dkt. Doto Biteko alisema hii leo Oktoba 31, 2023 kuwa Tanzania itanufaika na mkataba huo na itachangia kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na uharibifu wa mazingira na kuongeza kuwa malengo ya mkataba huo ni kuhamasisha matumizi endelevu ya nishati jadidifu.
Amesema, kuimarika kwa Nishati Jadidifu katika uzalishaji wa nishati ya umeme utaliwezesha taifa kuwa na vyanzo vya mchanganyiko wa umeme unaoendana na mahitaji ya ukuaji wa uchumi na jamii.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dkt. David Mathayo aliishauri Wizara kuhakikisha wataalamu wa kuzalisha Nishati hiyo wanapatikana ili kukidhi mahitaji.