Naibu waziri wa Nishati Stephen Byabato, amesema serikali itapitia upya mkataba wa kampuni ya kuzalisha umeme ya Songas, ili kuhakikisha kuwa haitakuwa na mkataba wenye dosari.
Naibu Waziri Byabato amesema hayo wakati akijibu swali la msingi bungeni jijini Dodoma, swali lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maluum Jesca Kishoa.
“Tayari Serikali kupitia TANESCO imeunda timu ya kupitia masuala ya msingi ya kuzingatiwa kwenye mkataba mpya kwa ajili ya maslahi kwa Taifa,” amesema Naibu Byabato.
Mkataba wa sasa kati ya serikali na kampuni hiyo ya Songas utaisha muda wake mwezi Julai mwaka 2024.
“Mkataba kati ya serikali na kampuni ya Songas utaisha muda wake mwezi Julai, 2024, ili kuhakikisha kwamba serikali inakuwa na mkataba usiokuwa na dosari serikali haitaongeza muda wa mkataba utakaoishia mwezi Julai, 2024.
Badala yake Serikali itajadili mkataba mpya na iwapo pande zote zitakubaliana mkataba mpya wenye tija kwa Taifa na usio kuwa na dosari utasainiwa,” ameongeza Naibu Waziri Byabato