Grace Mugabe ambaye ni mke wa Rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe ameeleza jinsi alivyoguswa na wema aliofanyiwa na Rais Emmerson Mnangagwa wakati wa msiba wa mama yake, ikiwa ni pamoja na kulipia gharama zote za mazishi.

Mke wa Mugabe alikuwa anatajwa kuwa hasimu mkubwa wa Mnangagwa aliyesababisha mumewe kumuondoa kwenye nafasi ya Umakamu wa Rais Novemba mwaka jana. Hali hiyo ilisababisha jeshi kushinikiza Mugabe kuachia madaraka na mwisho kumkabidhi Mnangagwa.

Mama Grace ameeleza kuwa Mnangagwa alikuwa binadamu kama yeye na kwamba alichomuonesha hivi sasa kimemgusa.

Alisema Rais huyo alimuandikia barua hivi karibuni ya kumpa pole akimuita ‘mama’. Na kusisitiza kuwa atahakikisha anagharamia mazishi yote ya mama yake, Idah Marufu aliyefariki mwishoni mwa mwezi uliopita.

“Rais aliniandikia barua na kunionesha upendo, alisema mimi ni mama yake na hataniangusha,” Grace anakaririwa na gazeti la Standard akiwaeleza waombolezaji Jumamosi iliyopita.

“Niliguswa na wema alionionesha. Ninawaambia leo, ni binadamu kama wewe na mimi. Tulijaribu kutumia fedha zetu, lakini Mnangagwa akatuambia tunzeni kiasi kidogo mlichonacho, tutawasaidia,” aliongeza.

Alisema kuwa wamepanga kukutana naye ili wamshukuru kwa kile alichowafanyia.

Hali hii imeonesha mabadiliko tangu Mnangagwa alipochaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo katika uchaguzi uliopata baraka za mahakama.

Mugabe ambaye alikuwa akionesha hasira dhidi ya Mnangagwa kwa namna alivyomuondoa madarakani, alibadili gia baada ya matokeo ya uchaguzi na kusisitiza kuwa wanamuunga mkono aliyeshinda.

“Wote tuna wajibu wa kuunga mkono Serikali. Tunasema kwa sasa mtu aliyeshinda ni Mnangagwa,” Mugabe alikaririwa na gazeti la Chronicle.

LIVE: Rais Magufuli katika uzinduzi wa daraja la mto Sibiti
Rais Bashir avunja baraza la mawaziri Sudan