Mke wa Rais wa Zimbabwe Grace Mugabe ametoa wito akitaka makamu wa Rais Emmerson Dambudzo Mnangagwa ambaye ana ushawishi mkubwa kutimuliwa kutoka katika chama cha Zanu-PF kabla ya mkutano wake wa mwezi ujao.

Grace Mugabe ameyasema hayo ikiwa ni siku moja baada ya Rais Robert Mugabe kutisha kumfukuza Mnangagwa ambaye ni makamu wa rais hatua ambayo imezua uvumi kuwa anataka mke wake amrithi.

“Nyoka ni lazima apigwe kwenye kichwa. Lazima tukabiliane na nyoka mwenyewe anayehusika na migawanyiko katika chama, tunaelekea kwenye mkutano tukiwa chama kimoja,” alisema Bi Grace Mugabe.

Rais Mugabe alimtaka Mnangagwa na wafuasi wake kumuonyesha uzalendo huku akisema kuwa hawezi kamwe kuvumilia matusi ya mara kwa mara kutoka kwa wafuasi wa makamu huyo wa rais.

Chama cha Zanu-PF kinatarajiwa kuifanyia mabadiliko katiba yake wakati wa mkutano na kuweka nafasi mbili za makamu wa rais moja ikiwa ni ya mwanamke nafasi hiyo ikitarajiwa kujazwa na Bi Mugabe na kuongeza uwezekano wa kumrithi mume wake.

Majaliwa ataka ujenzi wa shule ufanyike haraka
Picha: Taifa Stars yaanza mazoezi ya kuikabili Benin