Mke wa Rais wa Zimbabwe, Mama Grace Mugabe ameripotiwa kurejea nchini kwake na kuzika taarifa za jeshi la polisi la Afrika Kusini kuwa angejisalimisha kufuatia tuhuma za kumshambulia mrembo na kumjeruhi usoni.
Mwanamitindo wa Afrika Kusini mwenye umri wa miaka 20, Gabriella Engels alidai kuwa Mama Grace alimshambulia na kumjeruhi kichwani baada ya kumkuta kwenye chumba cha hoteli ya kifahari waliyofikia jijini Johannesburg akiwa na watoto wake wawili wa kiume, Robert na Chatunga.
Hata hivyo, Mama Grace au wawakilishi wake hawajazungumzia tuhuma hizo tangu zilipoibuliwa.
Afisa wa ngazi za juu wa Serikali ya Zimbabwe amekaririwa na Reuters akithibitisha kuwa Mama Grace amerejea nchini Zimbabwe.
- Mabilioni ya Escrow yaliyotoroshwa sasa kurejeshwa nchini
- Mbowe azidi kuweweseka na madiwani waliohama chama
“Ni kweli, amerejea nchini. Sisi hatufahamu hizo tuhuma za kumshambulia mtu zimetoka wapi,” alisema afisa huyo.
Awali, Jeshi la polisi nchini Afrika Kusini lilieleza kuwa lilikuwa likifanya makubaliano na wanasheria wa mke wa Mugabe ili aweze kujisalimisha polisi na baadae kufika mahakamani.