Sylvia Bongo, ambaye ni mke wa Rais aliyeondolewa madarakani nchini Gabon, Ali Bongo Ondimba amefunguliwa mashtaka ya utakatishaji fedha na makosa mengine, ikiwa umepita mwezi mmoja baada ya mapinduzi.
Sylvia ambaye ni raia wa Gabon na Ufaransa, sasa anau gana na mwanaye mkubwa, Noureddin Bongo Valentin, ambaye tayari amefunguliwa mashtaka ya rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma, pamoja na waliokuwa wajumbe wa Baraza la Mawaziri na Mawaziri wawili wa zamani.
Jaji mchunguzi, Andre Patrick Roponat alitangaza kufunguliwa kwa mashtaka hayo kwenye vituo vya Televisheni vya Serikali, huku akidai Mke huyo wa Ali Bongo ameamriwa kubaki katika kizuizi cha nyumbani jijini Libreville anapoishi tangu Agosti 30, 2023 akikabiliwa pia na mashtaka mengine ya kuficha na kughushi.
Ali Bongo mwenye umri wa miaka 64, aliitawala nchi hiyo ya Afrika ya Kati tangu mwaka 2009, hadi alipinduliwa na Viongozi wa Kijeshi Agosti 30, 2023 muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi katika uchaguzi wa rais.