Mke wa rais wa 41 wa Marekani, George H W Bush, mama Barbara Bush ambaye pia alikuwa mwanaharakati amefariki dunia.
Mama Bush ambaye pia ni mama wa rais wa zamani wa Marekani, George W Bush amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 92.
Taarifa ya kifo chake ilitolewa na ofisi ya rais, George H W Bush na ilieleza kuwa kifo chake kimetokana na matatizo ya kiafya.
Aidha, mara kadhaa mama Bush alilazwa hospitalini mara kwa mara ambapo siku ya Jumapili aliamua abakie nyumbani akiwa na familia yake.
Januari mwaka 2017, yeye na mumewe rais mstaafu Bush walilazwa kwa wakati mmoja. Yeye alikuwa akitibiwa kutokana na matatizo ya koo, huku mumewe akitibiwa kwa ugonjwa wa nimonia.
Hata hivyo, Mama Bush ni mmoja kati wanawake wawili tu nchini Marekani, kuwahi kuwa mke wa rais na mama wa rais. Abigail Adams alikuwa mke wa John Adams, na mama wa rais John Quincy Adams, rais wa sita wa Marekani.