Mke wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amefunguliwa mashtaka kwa tuhuma za ufisadi pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma.
Sara Netanyahu ameshtakiwa kwa kutumia vibaya $100,000 kwa kile alichodai ni fedha za kugharamia huduma ya chakula kwenye makazi ya Waziri Mkuu.
Pia, anatuhumiwa kwa kuvunja uaminifu dhidi ya jeshi la polisi kupitia mahojiano aliyofanya na jeshi hilo. Hata hivyo, Mama Sara alikana tuhuma zote dhidi yake. Mwanasheria wake alidai kuwa mashtaka hayo yamechochewa na hisia za kisiasa.
Jana, Mama Sara alifunguliwa mashtaka pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Ezra.
Mwanasheria wa Serikali wa wilaya ya Jerusalem alisema kuwa uamuzi wa kuwajumuisha washtakiwa hao kwenye kesi hiyo umetokana na mapitio ya ushahidi wote uliokusanywa.
Mwaka jana, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Avichai Mandelblit alitangaza kuwa anafikiria kumfungulia mashtaka mke wa Netanyahu kutokana na tuhuma zilizosababisha kufanyika kwa uchunguzi wa muda mrefu.
Kwa mujibu wa taarifa za kina, Mke wa Netanyahu na Seidoff wanatuhumiwa kutokana na utata wa gharama zilizotumika kati ya Septemba 2010 na Machi 2013, kwa ajili ya huduma za chakula kwenye makazi ya Waziri Mkuu ikiwa ni pamoja na kukodi wapishi maarufu.